Labels

Monday, June 11, 2012

UKITAKA NDOA YA RAHA, ACHANA NA BAADHI YA ULIYOYAPENDA

Wasaam wapenzi wa Blog hii,

Poleni kwa mapumziko mafupi ya mwishoni mwa wiki na karibuni tena katika ujenzi wa taifa letu changa na maskini. Tukitimiza wajibu siku moja mambo yatakuwa mswano tusijali!

Ama kwa hakika mengi yamejiri, huku ndugu zetu wakenya wakipoteza mawaziri na watumishi muhimu katika serikali yao kutokana na ajali ya helikopta-tunawapa pole nyingi kwa misiba hiyo, hapa kwetu Bongo tumekumbwa na msiba wa mzee wetu ambaye ni mmojawapo wa waanzilishi wa chama kimoja cha siasa mzee Bob Makani, poleni kwa wafiwa na Mungu mwingi wa rehema amsamehe na kumpokea kwake mbinguni.

Huku waheshimiwa wengine wakiuza sera Jangwani wengine walikuwa katika operation maalum mikoa ya kusini. Kama hayo hayatoshi kwa upande wa tasnia ya habari-michezo timu yetu ya taifa imetupa matumaini baada ya kuibuka kidedea dhidi ya timu ya Gambia kwa mabao mawili kwa moja- Viva Taifa Stars, keep it up! Huko Warsaw ndugu zetu waandamanaji nao vurugu tupu na polisi wakipinga mashindano ya EURO yanayoendelea!

Basi kabla ya kuchoshana katika soma soma magazeti wiki end hii nilikumbana na makala moja katika kona ya mahaba ya gazeti moja la kila siku ambayo natumaini itakuwa na manufaa kwa wasomaji wangu kwani inagusa kabisa lengo la msingi la Blog yetu.

Mwandishi huyu anasema UKITAKA NDOA YA RAHA, ACHANA NA BAADHI YA ULIYOYAPENDA! Ingawa hata hivyo kichwa hicho cha habari kilikosewa na kuandikwa ndo badala ya ndoa!

Anaanza kwa kuuliza, Je katika mahusiano yako mnaishi kwa raha au ili mradi siku zinakwenda mbele? Anaendelea kwa kubainisha kwamba hakika jibu utakuwa nalo mwenyewe. Lakini anatahadharisha kwamba huna budi kufahamu kuwa kama humpi raha mwenzi wako utakuwa unauharibu uhusiano wako wewe mwenyewe.

Mwandishi anaendelea kukumbusha yafuatayo katika mahusiano:-
1. Hakuna anayeingia katika mahusiano kutafuta matatizo, kama wapo ni wachache sana na watakuwa na matatizo nadhani wao wenyewe, hakuna anayetaka mahusiano ili atukanwe ama kupigwa.
2. Hakuna mwanaume ama mwanamke anayeingia katika mahusiano ili kupata mtu wa kumdharau.
3. Hakuna mtu anayeingia katika mahusiano ili kumpata mtu aliyekuwa busy na simu ama akichat au kuzungumza wakati wote bila kumjali.

Mwandishi huyu anaelewesha zaidi kwa kusema kwamba katika maisha yatupasa kufahamu kwamba tunapaswa kufanyiana mambo mazuri ili nasi tutendewe mazuri ni kosa kutarajia mazuri wakati unayotenda kwa wenzako si mazuri.

Watu wanaingia katika mahusiano kwa lengo la kusaka marafiki wema katika maisha yao. Watu wanatafuta wenza ambao watawasikiliza na kuwapa kipaumbele wao.

Mwandishi anatahadharisha kwamba kuna wanaume wengi wamesoma ama wana mali zaidi ya wake zao, lakini matokeo yake wanaendekeza dharau kwa wake zao, anasema huu ni upuuzi na kushauri kujaribu kuwa na hekima katika maisha, kwamba baraka unazopata zisiwe sababu ya kuharibu uhusiano wenu, anaendelea kutoa mfano wa wale wanaopanda vyeo na kutaka kuwaacha wale ambao walikuwa nao mwanzoni wakiona kwamba hawana hadhi ya kuwa nao. Mwandishi anasema haya si maisha ndugu zangu, ni vizuri kuheshimu wale ambao walitupenda tukiwa hatuna kitu.

Kama unaona anaonekana si mwenye kupendeza basi fanya uwezalo ili naye apendeze, hakuna mtu asiyependa kupendeza, zungumza nae, hakika atabadilika na kuwa mzuri zaidi. Cha msingi katika maisha ni kutoa nafasi ya kuzungumza na kusikilizana.

Mwandishi ameendelea kutahadharisha mambo ambayo hatuna budi kuyaepuka, kuyaacha ama kupunguza baada ya kuwa na mahusiano ili kuweza kulinda mahusiano yetu na kuyafurahia.
Mambo hayo ni kama:-

1. Marafiki - yatupasa kuangalia aina za marafiki tuliokua nao kabla ya mahusiano na faida tunazopata tokana na urafiki wetu, hatuna budi kutafakari na kuwachuja kulingana na umuhimu wa mahusiano husika. ni muhimu kuweka uwazi na ukweli zaidi kwa mwenzako kuhusu aina ya marafiki utakaoendelea kuwa nao. hata hivyo unashauriwa kupunguza kasi ya mawasiliano na marafiki hasa wa jinsia tofauti na hii inatokana na ukweli kwamba walio katika ndoa hawapendi kuona wenza wao wakiwa karibu na uhusiano wa jinsia tofauti zaidi yao. Kama unaendelea sana na ukaribu na mtu wa jinsia tofauti, tarajia kelele nyingi na ugomvi katika mahusiano yako.

2. Pamoja na kwamba ni muhimu sana kujenga tabia ya kuaminiana katika mahusiano lakini mwandishi anatukumbusha kwamba ni muhimu na vizuri kujenga hali na mazingira ya kuaminiwa.
Yeyote ambaye anahisi mwenzi wake hamwamini anapasa kujiuliza ni kwa nini haaminiwi? Wengi ni wepesi wa kukasirika lakini ni ujinga kukasirika unaposemwa na kuonekana si mwaminifu, bali unapaswa kupata muda na kutafakari sababu za msingi za kuonekana si mwaminifu.

Mwandishi anamalizia kwa kushauri kwamba urafiki mwingine ni wa kinafki hivyo yatupaswa kuwa makini unapotiliwa mashaka na mwenzi wako usikurupuke na kupayuka ama kugombana bali tafakari na kutumia wasaa mzuri kujieleza ukweli, utaeleweka.

Mwandishi huyu namalizia kwa kuuliza je mwenzi wako ni mlevi mno, nini kifanyike?
Je una mke ama mume mlevi, mwandishi anashauri hatua za mapema kuchukuliwa ili kuweka tahadhani na kushauriana ili kurekebishana mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.

Basi mwandishi wetu anamalizia kwa kushauri kwamba ukitaka ndoa ya maana, achana na baadhi ya uliyoyapenda kama vile baadhi ya marafiki kama si wa lazima.

Wakati nawatakia wiki yenye mafanikio, naahidi kuzungumzia hapo mbeleni tabia nyingine kadhaa ambazo yatupasa kuzingatia ama kuepuka ili kuwa na mahusiano yenye furaha.

Wasalaam.

No comments:

Post a Comment