Labels

Friday, June 8, 2012

Mfano wa kuigwa wa mahusiano kwa wasanii..

Ni kweli kwamba katika kila mahusiano kuna changamoto zake , kutokana hasa na mazingira ya mahusiano husika lakini kama makala moja ya kiingereza ambayo ilitangulia katika Blog yetu inavyosema ni kwamba changamoto hizi ndiyo kipimo hasa cha mahusiano yenyewe.

Ni jambo lililo wazi na linalofahamika kuona ama kusikia wasanii na watu maarufu mbalimbali wakitia aibu katika mahusiano yao ama kwa kutotulia ama kutokuwa waaminifu ama kushindwa kutunza na kujenga heshima ya mahusiano husika.

Ni kweli pia kwamba watu hao matatizo yao kimahusiano hufahamika zaidi kwa sababu ya nafasi zao katika jamii, umaarufu! Ndiyo, umaarafu una gharama zake, mojawapo ni hii ya kumulikwa kila wakati, kwani wao huchukuliwa kama kioo cha jamii!

Sisemi kwamba ni wasanii wote ambao wamekuwa na matatizo katika mahusiano yao, la hasha ila ukweli ni kwamba wengi wao wameshindwa kustahimili mikiki ya changamoto za mahusiano ama wametumia vibaya nafasi zao za umaarufu katika jamii kujirundikia viburudisho! Wakiona umaarufu kubadilisha wapenzi kila leo!

Katika maisha hakuna jambo jema na lenye ufahari kama jamii itakuchukulia kama mfano wa kuigwa kwa mambo ama mafanikio mbalimbali uliyopata na hata katika mahusiano yako. Mahusiano yenye maelewano, utulivu, amani, heshima na upendo.

Zipo faida nyingi sana za kuwa na mahusiano bora  kama niliyotaja hapo juu, kwa mfano: kuwa mfano bora katika jamii na hivyo kuheshimika, kupata mafanikio katika kazi na maisha kutokana na utulivu uliopo na amani katika mahusiano na pia mara nyingi hupelekea kujenga na kuwa na familia bora yenye amani na furaha.

Bahati mbaya hasara za mahusiano machafu nazo ni nyingi pengine kuliko faida. Mojawapo ikiwepo kujivunjia heshima na kuifanya jamii kukuchukulia kama mcharuko tu, kukosa mafanikio katika maisha kwani leo hapa kesho kule, mipango haiendi, kuwa na mafarakano mara kwa mara kutokana na kuchanganya wapenzi ama hata kutembea na wake ama waume za watu na mbaya na kubwa zaidi ni kupata magonjwa mbali mbali ikiwemo ukimwi.

Haya tumeyaona hapa kwetu Bongo, na mifano ni mingi sana, ingawaje wako wachache pia wenye kustahili pongezi na pia ni mifano ya kuigwa na jamii kwa utulivu walioonyesha katika mahusiano yao. Changamoto iliyopo ni kwa wasanii na watu maarufu wote kuhamasika na kubadilika, kujaribu kweli kuwa kioo cha jamii na kuwa mfano wa kuigwa badala ya kuwa wao ndiyo kichocheo cha matatizo na maporomoko ya maadili katika jamii husika.


 Ni aibu kubwa leo kusikia watu wakiongelea kama sifa, sijui mwanafunzi fulani anatoka na kigogo fulani, msanii yule kajengewa nyumba na boss fulani, mwalimu huyu antembea na yule?! Tubadilike, tutulie na kuwa mfano wa kuigwa!

Pamoja na kwamba Beyonce na mumewe Jay Z wako katika level nyingine kimaisha, kisanii lakini nimependa kuwachukulia kama mfano wa kuigwa kidunia, hapa tuna mwanaume na mwanamke "maarufu", hatuna jini au malaika, kwanini wengine washindwe?! Ni kweli kwamba kwangu mimi wao ni pendeleo langu la kwanza kimahusiano kama wasanii maarufu waliotulia lakini naamini kwamba watakuwa ni pendeleo la wengi.

Kinashindikana nini? Be responsible, play your part, kamata mupenzi wako mmoja na tulizana. Once you are in a relationship-respect it, take care of it!

Kwaheri for now!



No comments:

Post a Comment