Happy Blue Monday kwenu nyote na kila la kheri katika kuijenga nchi yetu na maisha binafsi kwa kila mmoja wetu.
Tukianza wiki mpya na mwezi mpya, nawapa pole ndugu zetu wa Kenya kwa mashambulio yanayoendelea dhidi yao, Mungu awalinde.
Poleni wapenzi wa Italia kwa kapu la magoli katika Fainali za kombe la mataifa ya Ulaya zilizomalizika jana, hakika timu ya Hispania ilistahili kuwa mabingwa! 4-0!
Wapendwa wataalam wetu wa tiba na hasa madaktari, kauli ya mkuu mtakuwa mmeisikia, chonde chonde tuweke utaifa mbele kwa maslahi ya maskini na wale wanaoteseka zaidi na walio wengi.
Wiki hii basi nitaendele na tafsiri zetu za misingi bora kwa mahusiano na ndoa bora!
UAMINIFU KATIKA MAHUSIANO..
Uaminifu ni msingi wa mahusiano yenye ukaribu, salama na ya mafanikio. Uaminifu ni lazima upatikane kwa stahili, uenziwe na kulindwa na uwe wa kudumu!
Kujenga uaminifu na kuamini kwamba mpenzi wako ni mwaminifu
kwako siyo mambo rahisi hasa kwa wale ambao wamewahi kusalitiwa uaminifu wao.
Hili ni tatizo kubwa katika jamii zetu kwani kusalitiana limekuwa jambo la kawaida!
Pale imani yako inapo vunjwa inakuwa vigumu kuweza kuwepo
tena katika mahusiano yako. Makala hii itakusaidia kuelewa njia ambazo
zitakusaidia kurudisha imani hiyo.
Uaminifu lazima uwe jambo la kila wakati na siku zote ili
mahusiano yaweze kudumu.
Uaminifu ni muhimu katika mahusiano ya aina zote uwe wa
mapenzi, kifamilia na hata katika urafiki wa kawaida.
·
Kwa kuanzia, kuwa katika mahusiano ya kimapenzi
kuna faida nyingi kwa mwili, watu walio katika mahusiano bora ya mapenzi huishi
maisha marefu na kufurahia afya njema kuliko wale wasiokuwa katika mahusiano ya
aina hiyo. Faida hii haina pingamizi kwa sababu ya ukweli kwamba watu wanaokuwa
katika mahusiano ya karibu wanajijengea
hisia na nguvu fulani ambayo huwasaidia kusaidiana na kujaliana wakati wa
shida. Siyo tu kwamba watu walioko katika mahusiano ya aina hii wanaishi muda
mrefu lakini pia ni kweli kwamba wanakuwa na furaha na wanaridhika na maisha
kuliko wale wanaoshindwa kukaa katika mahusiano.
·
Pili, kuwa katika mahusiano mazuri ya mapenzi
kunasaidia katika mambo mbalimbali ya kimahitaji. Kusaidiana katika mahitaji
mbalimbali baina ya wapenzi ni njia nzuri ya kuwa na maendeleo. Watu wawili
wanaoshirikiana pamoja mara nyingi watakuwa na maisha mazuri zaidi ya yule anayefanya
peke yake. Unapokuwa na mtu karibu wa kusaidiana naye katika mahitaji ni rahisi
kupata mafanikio.
· Tatu, Watu walio katika mahusiano mazuri
wanapata msaada wa kijamii; kwa maana ya kuwa na mtu karibu ambaye anajali
mahitaji yako ya msingi na hisia zako. Kuwa na msaada wa aina hii kuna faida
nyingi, mojawapo muhimu ni kuweza kufanya maamuzi ya busara bila kuwa na mtindio wa mawazo na hofu ama
mashaka.
· Nne, kuwa na mwenza katika maisha hufanya maisha
kuwa ya faraja zaidi. Kuwa na mtu ambaye mnaweza kushirikiana mambo madogo madogo
ya maisha kama kuangalia Tv, kutembea, kula pamoja ni muhimu; inaboresha mahusiano
na mara nyingi watu walio katika mahusiano ya aina hii wamekuwa na maisha bora
zaidi.
· Tano,
Mahusiano ni muhimu kwa sababu wapenzi wana kawaida ya kuangaliana tabia zao
hasa zile ambazo ni haribifu, na wamekuwa na kawaida ya kuonyana ama kushauriana
kuacha kufanya mambo mabaya na tabia mbaya. Kwa mfano watu walio katika mahusiano
ya karibu wamekuwa na tabia ya kujaribu kuwashauri wapenzi wao kuacha kuvuta
sigara, kupunguza pombe, kuacha kutumia madawa ya kulevya nk.
· Mwisho, Watu walio katika mahusiano bora ya
kimapenzi wanafanya mapenzi mara nyingi zaidi kuliko wale walio pekee. Kufanya mapenzi
mara kwa mara, kimpangilio ni muhimu kwa afya bora ya mwili na akili. *Ni
muhimu kuzingatia kwamba kufanya huko mapenzi ambako ni bora kwa afya ya mwili
siyo kubadilisha wanaume ama wanawake, ila ni kwa mwenza wako ama mke au mume
na katika hali ya maelewano, uhuru na amani lakini pia kwa utaratibu
unaostahili ndiyo upelekea kuleta faida hiyo.
Baada ya kusema yote hayo, ni
ukweli kwamba mahusiano mazuri baina ya wapenzi huwa na faida nyingi kwa watu
wenye bahati ya kupata mtu wa kumpenda na hatimaye nao kupendwa pia.
Hatua muhimu katika
kujenga uaminifu zitafuata…